UBORA WA KUISHI NA WATU VYEMA

SIKU moja, kijana mmoja akitokea mihangaikoni, alimwona Mama fulani akiwa amesimama nje ya gari yake, pembezoni mwa barabara. Licha ya giza la usiku, kijana aliweza kugundua Mama yule yuko taabuni akitarajia msaada. Kijana alijiweka tayari kutoa msaada na kumsogelea.
Pamoja na bashasha usoni mwa kijana, bibi alijawa na hofu juu ya usalam wake. Kwa takribani saa kadhaa alizokwama mahala pale, hakuna aliyesimama kumsaidia. Hivyo, kwa ujio wa kijana yule, mwenye haiba ya njaa na mchoko wa umasikini, bibi alibaki njia panda. Hakujua endapo atapata msaada au madhila. Baada ya salaam, kijana alijitambulisha: "Ninaitwa Rama Mgonja. Nimekuja kukusaidia tu, ondoa hofu."
Tatizo la gari halikuwa kubwa - tairi lilikuwa na pancha - japo kwa mama wa makamo kama yale, lilikuwa ni tatizo kubwa. Bila kurefusha muda, Rama akaingia uvunguni mwa gari ili kuipachika uzuri jeki. Ndani ya dakika chache tu, tayari akalitoa tairi bovu na kufunga zima. Zaidi ya kuchafuka kidogo tu mikono na nguo zake, hakuna kingine alichopoteza.
Baada ya zoezi kumalizika, mama Yule aliingia ndani ya gari na baada ya kuketi, alifungua pochi yake na kutoa pesa, takribani shilingi laki moja, kisha akasema: "Rama, umenifaa sana mwanangu. Zaidi ya shukrani, naomba nikupe kiasi hiki cha pesa kama ahsante yangu."
Hata kwa mwonekano wake tu - pesa haikuwa tatizo kabisa kwa mama yule; Vito alivyovaa, gari anayotumia, manukato anayonukia, vyote vilidhihirisha dalili za ughali wa maisha yake. Pamoja na hayo, Rama alikataa: "Usijali mama. Sikuja kufanya kazi, nilikuja kutoa msaada. Jukumu la kutoa malipo kwa mtu aliyeamua kujitolea msaada kwa mwenye uhitaji, ni la Mungu mwenyewe."
Mama alipigwa butwaa. Hakuwahi kukutana na kijana mwenye moyo wa namna ile, pamoja na kuoneshewa pesa. Hivyo ndivyo Rama alivyo - na amekuwa akiishi katika utaratibu huo karibu maisha yake yote. Rama akaongezea kusema: "Kama unahitaji kunilipa kwa dhati, basi siku yoyote utakapokutana na mtu mwenye uhitaji, msaidie kwa niaba yangu."
Baada ya kuagana na kutakiana kila la kheri maishani, Rama alirejea nyumbani kwake akiwa mchovu kiasi, huku yule mama akiendelea na safari yake. Baada ya kuendesha kwa kitambo kidogo, mama aliamua kuegesha nje ya kiji-amgahawa kidogo kilichokuwa kando mwa barabara, na kuingia. Mhudumu wa kike alimlaki kwa bashasha, na kuomba kumhudumia kwa utii na taadhima kubwa. Mama aliagiza chai na sambusa.
Baada ya mhudumu kuleta alichoagizwa na kuondoka, mama aligundua kwamba, mhudumu yule alikuwa na ujauzito upatao miezi tisa. Yu mbioni kujifungua. Lakini kwa uchovu aliokuwa nao, bila shaka adha za kimaisha ndizo zilizomfanya aendelee kujishughulisha. Bila shaka alihitaji msaada. Mama akakumbuka ahadi waliyowekeana na Rama - kumsaidia mtu mwenye uhitaji, kwa niaba yake.
Baada ya kumaliza kula, Mama alimwita mhudumu na kumlipa noti ya shilingi elfu kumi. Upesi mhudumu aliondoka kwenda kumchukulia chenji yake. Mhudumu aliporejea mezani na chenji, alikuta mama amekwisha kutoweka. Akiwa anatafakari mahala alipokwenda Mama yule, mhudumu aliona karatasi juu ya meza ikiwa imeandikwa. Machozi yalimbubujika baada ya kuusoma ujumbe ule ulioandikwa kama hivi: 'Nimeiona shida ya ujauzito unayopitia. Unajaribu kuchangamkia wateja, unajilazimisha na kujibidiisha kufanya kazi, ili kujipatia chochote cha kujikimu, lakini maungo hayataki - uchovu umetamalaki. Kwa hakika unahitaji msaada. Huko nilikotoka kuna mtu amenisaidia kwa kunibadilishia tairi la gari bila kudai malipo. Msaada alionipa ndo umenisukuma nami kukusaidia wewe. Nawe usiache kusaidia mwingine mwenye uhitaji - dunia itakuwa mahala salama pa kuishi.'
Pamoja na barua hiyo fupi, mama aliacha mezani viji-bunda viwili vya pesa - shilingi milioni mbili. Unafikiri kazi ilifanyika tena? Mhudumu alikusanye vitu vyake na kuondoka akiwa amepagawa kwa furaha.
Alipofika nyumbani, alimkuta mumewe amejilaza kitandani. Kabla hajampa habari njema ya zile pesa, aligundua kitu. Mumewe alikuwa amechafuka nguo na mikono. Akamuuliza: "Mbona umechafuka hivyo?"
Mume akajibu, "Huko njiani kuna Mama aliharibikiwa gari, nikaamua kumsaidia kubadili tairi."
"Mungu wangu," mke alimaka, "kumbe ni wewe ndo ulimsaidia yule mama? Siamini Rama!"
Rama akabaki ameduwaa asielewe kisa wala mkasa. Huku akibubujikwa machozi ya furaha, mke alimsimulia mumewe kisa chote. Kukubali kutoa msaada kidogo, kumepelekea kupatikana pesa nyingi kwa ajili ya familia. Pengine Rama angeipokea ile laki moja, asingeipata hiyo milioni mbili. Basi kila mwenye akili na ajifunze.
Nikutakie Siku njema.

Si vibaya ku-share ujumbe huu ili kila aupataye huenda akawa ni miongoni mwa watakaotoa kwa wenye uhitaji. TUPANDE WEMA TUVUNE MEMA!!!

Commentaires

Posts les plus consultés de ce blog

VITA VYA DUNIA HISTORIA YA MBAVU MOYA

Unakaribishwa we mgeni wa ulimwengu wa mtandao

Zijuwe sharti za google adsense