Anza biashara yako kwa mtaji mdogo
Nimemalza chuo mwaka jana sijaajiriwa, nina ndoto za kujiajiri lakini mpaka sasa nmefanifakiwa kupata lak 3 so sjui nianzie wapi na nianze na lipi kwa huu mtaj maana kukodi frem tu ni elf 30/mwez na wanahtaj miez 6
Nahitaji kufanya biashara, na nimeshaanda mtaji kiasi kama cha millioni 2 . Tatizo langu nashindwa nifanye biashara gani na nianze vp? Naomba msaada wako.
Ni mradi, miradi gani nianzise kwa mtaji wa laki mbili?
Hayo ni baadhi tu ya maoni mengi ambayo nimepokea kuhusu changamoto ya biashara gani ya kufanya hasa mtu anapokuwa na mtaji kidogo.
Kitu kikubwa ambacho mpaka sasa nimejifunza kutokana na mawasialiano na watu wengi ni kwamba wengi wanaamini kwamba ukishakuwa na mtaji tu na ukapata wazo zuri la biashara basi mafanikio yako nje nje. Ni kutokana na imani hii watu wengi wanaomba sana kusaidiwa ushauri kwamba wafanye biashara ya aina gani.
Kama nilivyowahi kusema kwamba sababu ya mtaji ni kisingizio tu cha kutokuwa tayari kuingia kwenye biashara, na hii ya kufikiri kuna wazo bora la biashara ambalo ukilijua tu umeshafanikiwa ni kisingizio kingine kwa watu ambao hawajawa tayari kuingia kwenye biashara.
Ni kweli kwamba kuna baadhi ya biashara ni nzuri sana na zinapata faida kubwa. Ila katika bishara hizo kuna watu ambao wanafanikiwa sana na kuna wengine wanapata hasara kubwa. Pia zipo biashara ambazo zinaonekana ni mbaya na hazina faida kubwa, ila pia katika biashara hizi kuna watu ambao wana wanafanikiwa sana na kuna wengine wanapata hasara kubwa.
Hivyo basi kinachosababisha mtu kufanikiwa kwenye biashara sio aina gani ya biashara anayofanya.
Ni kitu gani hasa kinaweza kumletea mtu mafanikio kwenye biashara yoyote na je uanzie wapi?
Kwanza kabisa anzia hapo ulipo. Anza kwa kuangalia ni kitu gani unapenda kufanya au unapenda unapoona watu wanakifanya. Pia angalia mazingira yanayokuzunguka watu wanakosa nini au kuna biashara gani ambazo hazijatumika vizuri kwenye eneo hilo. Baada ya hapo chagua biashara moja ambayo utaingia na kisha jipange kweli kwa ajili ya kufikia mafanikio.
Ni mambo gani ya kufanya ili ufikie mafanikio kwenye biashara yoyote?
Baada ya kuamua ni biashara gani unafanya, kuna mambo muhimu unatakiwa kufanya au kuwa nayo ili kujihakikishia mafanikio. Mambo hayo ni;
1. Kuwa na malengo na mipango. Bila ya malengo ni vigumu sana kufikia mafanikio makubwa. Bila ya mipango huwezi kujua ni kipi ufanye na kipi uache kufanya.
2. Jitoe kweli kwenye biashara hiyo. Jitoe moja kwa moja kwenye biashara yako, jipange kutumia kila nguvu na ujuzi wako katika biashara hiyo. Amua kufanya kwa viwango vya juu sana na kuwa na ubunifu mkubwa tofauti na wengine wanavyofanya.
3. Fanya kazi kwa bidii na maarifa. Fanya kazi sana, mwanzoni mwa biashara unaweza kufanya kazi zaidi ya masaa kumi na mbili kwa siku, huna njia ya kukwepa hilo, kazi ni muhimu sana.
4. Kuwa mvumilivu. Hata ungeanza biashara na mtaji wa milioni 100 bado utakutana na changamoto nyingi sana. Ukweli ni kwamba kila biashara ina changamoto zake na kuna kipindi unaweza kuona kama ndio mwisho na huwezi kusonga tena mbele. Usikubali kukata tamaa, kuwa mvumilivu na siku sio nyingi utafikia mafanikio makubwa.
5. Jifunze sana, jifunze kila siku. Kama haupo tayari kujifunza kila siku naweza tu kukushauri usiingie kwenye biashara. Kwa sababu kama hutajifunza kila siku utakuwa unafanya biashara kwa mazoea kitu ambacho kitakufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa. Jifunze kwa kusoma vitabu, kuhudhuria semina mbalimbali na hata kwenye mitandao kama hii AMKA MTANZANIA. Pia jiunge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo utajifunza zaidi kuhusu biashara na ujasiriamali, tabia za mafanikio na hata kupata uchambuzi wa vitabu.
Wakati mwingine utakapojiuliza nifanye biashara gani kwa mtaji huu kidogo nilionao tafadhali tumia ushauri huu niliotoa hapa. Mafanikio katika biashara hayatokani na ni aina gani ya biashara unafanya, bali yanatokana na wewe mwenyewe ni jinsi gani unafanya biashara hiyo. Tayari umeshajua ni namna gani ya kufanya biashara ili ufanikiwe. Fanya hivyo ili uweze kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
Commentaires